NANI ANASEMA POSHO YA SH 300,000 KWA SIKU HAZITOSHI BUNGE LA KATIBA


Hata kabla ya kupita wiki moja tangu Bunge Maalumu la Katiba kuanza rasmi shughuli zake, wajumbe wake wameendelea na vituko kiasi cha kutupa wasiwasi kama kweli wengi wa wajumbe hao wanastahili kutuwakilisha katika chombo hicho kufanya kazi ya kihistoria ya kutunga Katiba Mpya. Tulisema jana kupitia safu hii kwamba wengi wa wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba hawaonyeshi kama kweli wanatambua nafasi na hadhi waliyonayo kama wawakilishi wetu katika chombo hicho, kwani vitendo na kauli zao vinajenga picha tofauti. Ndiyo maana tulionya kwamba Bunge linapoanza shughuli zake kwa kutawaliwa na vioja na vituko haliwezi kamwe kufikia malengo yaliyokusudiwa.

Ni jambo la kusikitisha kuwa, pamoja na angalizo letu kwa wajumbe wa Bunge hilo, jana na juzi tulishuhudia mwendelezo wa vitendo vya aibu ambavyo kwa vyovyote vile siyo tu vimekidhalilisha chombo hicho, bali pia vimeibua maswali mengi miongoni mwa wananchi ambao wamehoji kama kweli Bunge hilo limeundwa na watu wenye sifa na hadhi ya kuitwa wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba. Kilele cha vioja na vitimbi hivyo ni pale wajumbe wengi walipozusha zogo mithili ya watoto wa chekechea kwa madai kwamba posho ya Sh300,000 wanazopewa kila siku hazitoshi na badala yake wanataka wapewe Sh420,000.

Ni kichekesho cha karne kwamba akili za wajumbe wengi, badala ya kuelekezwa kwenye ufanisi wa shughuli za Bunge hilo kama kudai wapewe makabrasha yenye nyaraka zilizoandaliwa vizuri au nakala za kutosha za Rasimu ya Mabadiliko ya Katiba pamoja na Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, zimeelekezwa kwenye fedha na kuchumia matumbo yao. Tayari wamesahau kwamba waliteuliwa kuingia katika Bunge hilo kujitolea na kujitoa mhanga ili kuhakikisha inapatikana Katiba Mpya na siyo kugeuza uwakilishi wao katika Bunge hilo kuwa ajira.

Kichekesho kingine ni kwamba madai hayo ya kipuuzi waliyatoa wakati wa semina waliyoandaliwa kwa ajili ya kupatiwa rasimu ya Kanuni zitakazoongoza shughuli za Bunge. Badala ya kuzungumzia rasimu hiyo, wajumbe walilifanya suala la posho kuwa kipaumbele chao na kutaka walipwe viwango vya posho kama makamishna wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba walivyolipwa, huku wakipuuza ukweli kwamba makamishna hao na madereva wao walistahili kulipwa viwango hivyo kwa sababu walisafiri nchi nzima, tena katika mazingira magumu na kufanya kazi usiku na mchana. Uzoefu wetu umetuonyesha kwamba wengi wa wajumbe wa Bunge hili watatumia muda mwingi kuchapa usingizi au kukacha vikao. Ndiyo maana wanataka walipwe posho hata wasipohudhuria vikao.

Kwa sababu ya woga usiokuwa na msingi wowote, uongozi wa Bunge umesikiliza upuuzi huo na kuteua kamati ya watu sita eti kwenda kuona ugumu wa maisha ulivyo mitaani. Badala ya kusimamia ukweli kwamba Sh300,000 ni nyingi sana kwa matumizi ya kila siku, uongozi wa Bunge na Serikali sasa utakuwa unaandaa mkakati wa kuongeza posho hizo. Hii ni kinyume na hali ya uchumi wa nchi yetu ilivyo, kwani Serikali imeelemewa na Deni la Taifa la zaidi ya Sh27 trilioni, kwa maana ya Sh20.23 likiwa deni la nje na Sh6.81 trilioni likiwa deni la ndani ambalo Serikali imeshindwa kulilipa. Tusisahau kwamba ukarabati wa Ukumbi wa Bunge umegharimu zaidi ya Sh8 bilioni.

0 comments: